Tunaendelea tena leo, kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.
Leo tunatafakari YOHANA 7:17-52. Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni,
“JINSI YA KULIELEWA NENO LA MUNGU“, kuna mengi zaidi ya kujifunza
katika mistari hii. Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika
mistari hii, katika vipengele kumi:-
(1) JINSI YA KULIELEWA NENO LA MUNGU (MST. 17);
(2) JINSI YA KUMTAMBUA NABII WA KWELI (MST. 18);
(3) KUSHINDWA KWA WANADAMU WOTE KUISHIKA TORATI (MST. 19);
(4) SABABU KUU YA KUMWITA MTUMISHI WA MUNGU KWAMBA ANA PEPO (MST. 19-20);
(5) WAJIBU NA JINSI YA KUHUKUMU (MST. 21-24);
(6) SABABU KUU YA WATU WENGI KUSHINDWA KUMPENDA MUNGU (MST. 25-29);
(7) SAA YA KUKAMATWA (MST. 30);
(8) NAMI NILIPO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 33-36);
(9) MITO YA MAJI YALIYO HAI (MST. 37-44);
(10) KOSA LA KUMHUKUMU MTU KABLA YA KUMSIKIA (MST. 31-32, 45-
52).
(1) JINSI YA KULIELEWA NENO (MST. 17)
Biblia, ni kitabu kinachochapishwa na kutolewa nakala nyingi sana na
kusambazwa na kusomwa kwa wingi, kuliko Kitabu chochote kile kingine
ulimwenguni, katika wakati wote na miaka yote. Kwa mfano, kulingana na
vitabu vyenye takwimu, “ENCYCLOPAEDIA BRITANNICA“ na “ENCYCLOPAEDIA
AMERICAN“, mwaka 1932 peke yake Biblia zilizoschapishwa na kusambazwa
kwa lugha mbalimbali duniani, zilikuwa 1,330,213,815. Miaka 50
iliyopita kulingana na mtafiti anayeitwa HY PICKERING, ili kukidhi
mahitaji ya Biblia, Chama cha Biblia cha BRITISH AND FOREIGN BIBLE
SOCIETY, kililazimika kuchapa nakala moja ya Biblia kila baada ya
SEKUNDE TATU mchana na usiku au karibu nakala 32,876 kila siku katika
mwaka mzima. Biblia hizi zilisambazwa katika ulimwengu mzima kwa
kutumia makasha 4,583 yenye uzito wa karibu TANI 500! Hata hivyo, jambo
la kushangaza ni kwamba mamilioni ya watu wanaosoma Biblia hawaielewi!
Tunajuaje kwamba hawaielewi? Maisha ya watu hawa hayabadiliki na
kufuata maelekezo ya Neno la Mungu. Tatizo ni nini? Jibu tunalipata
katika MST. 17 “MTU AKIPENDA KUYATENDA MAPENZI YAKE (MUNGU), ATAJUA
HABARI YA YALE MAFUNZO“. Kama mtu hayuko tayari kulitenda kila jambo
atakalofundishwa na Mungu katika Neno lake, Roho Mtakatifu humwacha mtu
huyo, hawezi kumfunulia chochote katika Neno la Mungu. Matokeo yake
hawezi kuelewa lolote! Bila roho Mtakatifu hatuwezi kufunuliwa na
kulielewa Neno la Mungu (1 WAKORINTHO 2:10, 13; YOHANA 16:13). Wengi
wetu hatulielewi Neno kwa sababu hatuko tayari kulitendas. Hatua yoyote
ya kushindana na kupingana na Neno la Mungu, humfanya Roho Mtakatifu
kutuacha mara moja. Kabla ya kulisoma neno au kujifunza Neno la Mungu
kwa njia yoyote, ili tulielewe Neno la Mungu, hatuna budi kuwa na
msimamo wa kutaka kulitenda Neno lake sawasawa na (YEREMIA 42:1-6).
(2) JINSI YA KUMTAMBUA NABII WA KWELI (MST. 18)
Yeye anenaye kwa nafsi yake tu, huyo siyo nabii wa kweli. Kunena kwa
nafsi yake mtu, ni kuhubiri au kufundisha kinyume na Neno la Mungu. Mtu
wa jinsi hii, hatafuti Utukufu wa Mungu, bali wake mwenyewe. Nabii wa
kweli humhubiri Kristo, au kwa jinsi nyingine, hulihubiri Neno!
(WAFILIPI 1:18; 2 TIMOTHEO 4:2).
(3) KUSHINDWA KWA WANADAMU WOTE KUISHIKA TORATI (MST. 19)
Wanadamu wote mble za macho ya Mungu, hakuna hata mmoja aliyeweza
kuishika torati, maana mtu akiishika sheria yote, ila akajikwaa katika
neno moja, anahesabiwa kukosa juu ya yote (YAKOBO 2:10). Hivyo, mbele
za Mungu, hakuna mwanadamu atendaye mema, la, hata MMOJA! (WARUMI 3:10,
12; 1 YOHANA 1:8). Wanadamu wote tulistahili kuangikwa msalabani kama
adhabu ya laana ya kutokuishika torati (WAGALATIA 3:10; KUMBUKUMBU
21:22-23). Aliyempendeza Mungu sikuzote, na kufanya yaliyompendeza, ni
Yesu Kristo pekee (MATHAYO 3:17; YOHANA 8:29). Ni kwa sababu hii,
tunahesabiwa haki BURE kwa neema yake, kwa neema yake, kwa njia ya
ukombozi ulio katika Kristo Yesu kwa imani katika damu yake iliyomwagika
msalabani, alipokufa kwa niaba yetu, ili awe upatanisho (WARUMI
3:24-26; 1 TIMOTHEO 2:5-6).
(4) SABABU KUU YA KUMWITA MTUMISHI WA MUNGU KWAMBA ANA PEPO (MST.19-
20)
Mtumishi yeyote wa Mungu anayeyafichua maovu yaliyo……………………………. katika
jamii ya watu wanaojiita Wakristo, na kuyanena waziwazi kwamba
hayampendezi Mungu, na kuisema kweli, huyu sharti watu hao watamwita ana
pepo. Dhambi zinapokubalika katika Kanisa lote la Mungu na watu
wanaojiita Wakristo, wanapokuwa hawana tofauti na wapagani au mataifa,
anapoinuliwa Mtumishi wa Mungu na kuleta mageuzi, sharti mtu huyo
ataitwa ana pepo. Yesu hapa alifichua maovu yao na kuisema kweli kwamba
wanataka kumuua, wao wakakana, wakaipinga kweli hiyo wakati ilikuwa
kweli; kinyume chake wakamwita ANA PEPO, ili kujikosa na kuhalalisha
maovu yao! (MST. 19-20, 23). Hivyo ndivyo inavyokuwa wakati awote.
Haya yalimpata Martin Luther, John Wesley, Charles Finney na wote
walioleta mageuzi ya jinsi hii nyakati zao.
(5) WAJIBU NA JINSI YA KUHUKUMU (MST. 21-24)
“Ifanyeni hukumu iliyo haki“, ni mafundisho ya Yesu Kristo kwetu.
Hatupaswi kukaa kimya kwa visingizio vya Neno, “Msihukumu“, na kuacha
kuyakosoa mafundisho potofu ya Mashahidi wa Yehova; Mormonism au Christ
Church for Latter Day Saints, wanaoshika mafundisho ya Joseph Smith; au
wanaojiita Wakristo na kusema wao siyo dhehebu, wanaofuata mafundisho ya
William Branham; au mafundisho yanayofundisha watu kushika sabato leo,
au mafundisho mengine yoyote yaliyo potofu. Kukaa kwetu kimya na
kuogopa “kuyasema madhehebu mengine“, siyo kufuata nyayo za Mchungaji
Mkuu wa Kondoo, Yesu Kristo na kufanya hivyo, ni kuwaachia kondoo wetu
wararuliwe na mbwa mwitu. Huo ni uchungaji wa mshahara. Yesu aliifanya
hukumu iliyo haki, pale alipokuwa kinyume na kuishika Sabato, na tena
pale aliposema “Jilindeni na *chachu* au mafundisho ya Mafarisayo na
Masadukayo“. (MATHAYO 16:11-12; YOHANA 10:12; MATENDO 20:28-30).
Tunapaswa kufuata kielelezo cha Yesu. Kanisa la Kwanza walizingatia
kufanya hivyo (WARUMI 16:17; 2 YOHANA 1:9-11). Watu wenye mafundisho
potofu, hatupaswi kuwa na ushirika nao, tuwahesabu tu kama mataifa na
kuwahubiria kweli na kutokukubali kusikia chochote kutoka kwao.
(1) SABABU KUU YA WATU WENGI KUSHINDWA KUMPENDEZA MUNGU
(MST.25-29)
Tangu zamani za kale, sababu kuu ya watu wengi kushindwa kumpendeza
Mungu, ni watu hao kuacha kumwamini Yesu na kuokolewa, kwa kungoja
kwanza WAKUU WAMWAMINI (MST. 26). Wengine wanangoja kwanza baba na
mama, mume au kiongozi wao wa dini aokoke, ndiyo eti nao waokoke, na
wanafuata mafundisho yao tu kimkumbo. Huu ni mtego mkubwa wa Ibilisi.
Ukitengwa ugali mezani kila mtu huchukua tonge lake mwenyewe! Ndivyo
ilivyo, damu imemwagika msalabani, wokovu tayari. Kila mmoja anapaswa
kuuchukua kwa imani. Ni muhimu kukumbuka pia kwamba, kila mtu
atalichukua furshi lake mwenyewe na kutoa habari zake MWENYEWE
(WARUMI14:12; WAGALATIA 6:5). Hakuna haja ya kungoja wakuu waokoke
ndiyo nasi tuokoke. Kufa hakufuati nani wa kwanza kuzaliwa!.
(7) SAA YA KUKAMATWA (MST. 20).
Maadui zetu watatutafuta sana ili watushike na kutudhuru, hata hivyo,
hatupaswi kuhofu. Hatuwezi kufa mpaka saa yetu itakapowadia. Juhudi
zao zitagonga mwamba, wakati wote Bwana wetu atatupa mlango wa kutokea
maana amesema atakuwa pamoja nasi hat ukamilifu wa dahari yaani mwisho
wa mambo yote (MATHAYO 28:19-20; AYUBU 5:20, 26-27).
(8) NAMI NILIPO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 33-36)
Hatuwezi kumwona Yesu pasipo Utakatifu na kutafuta kwa bidii kuwa na
amani na watu wote (WAEBRANIA 12:14). Ni wale tu wenye mioyo safi
watakaomwona Mungu (MATHAYO 5:8). Ikiwa tumejaa masengenyo, chuki,
fitina, hasira, mawazo machafu, n.k. tutamtafuta Yesu tusimwone.
(9) MITO YA MAJI YALIYO HAI (MST. 37-44)
Mtu akimpokea Roho Mtakatifu, ishara ya kwanza itakayoonekana kwake, ni
kunena kwa lugha mpya kadri roho atakavyomjalia kutamka (MATENDO 2:4;
10:44-46; 19:6). Maji yanapokuwa yanapita katika mto, hutoa aina fulani
ya sauti isiyoweza kuelezeka. Ndivyo alivyo mtu anenaye kwa lugha
baada ya kumpokea Roho, mito ya maji hutoka ndani yake!
(1) KOSA LA KUMHUKUMU MTU KABLA YA KUMSIKIA KWANZA NA KUJUA
ATENDAVYO (MST. 31-32, 45-52)
Watu wengi hufanya kosa la kumhukumu Mtumishi wa Mungu kabla ya kumsikia
kwanza anenavyo au anavyofundisha na kujua atendavyo. Haitupasi
kufanya hivi. Watumishi waliotumwa na makuhani kumkamata Yesu,
walikubali kwanza kumsikia na wakagundua kweli waliyokuwa wamefichwa na
Shetani. Kuna faida kubwa kuiga mfano wao.
…………………………………………………………………………………………………………………………………. .
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA
12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO
WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu
ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa
kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata
rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko
tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi
fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante
kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili
kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.
Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe.
Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji
umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka
siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa
linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment