Tunaendelea tena leo, kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.
Leo tunatafakari YOHANA 7:17-52. Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni,
“JINSI YA KULIELEWA NENO LA MUNGU“, kuna mengi zaidi ya kujifunza
katika mistari hii. Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika
mistari hii, katika vipengele kumi:-
(1) JINSI YA KULIELEWA NENO LA MUNGU (MST. 17);
(2) JINSI YA KUMTAMBUA NABII WA KWELI (MST. 18);
(3) KUSHINDWA KWA WANADAMU WOTE KUISHIKA TORATI (MST. 19);
(4) SABABU KUU YA KUMWITA MTUMISHI WA MUNGU KWAMBA ANA PEPO (MST. 19-20);
(5) WAJIBU NA JINSI YA KUHUKUMU (MST. 21-24);
(6) SABABU KUU YA WATU WENGI KUSHINDWA KUMPENDA MUNGU (MST. 25-29);
(7) SAA YA KUKAMATWA (MST. 30);
(8) NAMI NILIPO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 33-36);
(9) MITO YA MAJI YALIYO HAI (MST. 37-44);
(10) KOSA LA KUMHUKUMU MTU KABLA YA KUMSIKIA (MST. 31-32, 45-
52).
(1) JINSI YA KULIELEWA NENO (MST. 17)
Biblia, ni kitabu kinachochapishwa na kutolewa nakala nyingi sana na
kusambazwa na kusomwa kwa wingi, kuliko Kitabu chochote kile kingine
ulimwenguni, katika wakati wote na miaka yote. Kwa mfano, kulingana na
vitabu vyenye takwimu, “ENCYCLOPAEDIA BRITANNICA“ na “ENCYCLOPAEDIA
AMERICAN“, mwaka 1932 peke yake Biblia zilizoschapishwa na kusambazwa
kwa lugha mbalimbali duniani, zilikuwa 1,330,213,815. Miaka 50
iliyopita kulingana na mtafiti anayeitwa HY PICKERING, ili kukidhi
mahitaji ya Biblia, Chama cha Biblia cha BRITISH AND FOREIGN BIBLE
SOCIETY, kililazimika kuchapa nakala moja ya Biblia kila baada ya
SEKUNDE TATU mchana na usiku au karibu nakala 32,876 kila siku katika
mwaka mzima. Biblia hizi zilisambazwa katika ulimwengu mzima kwa
kutumia makasha 4,583 yenye uzito wa karibu TANI 500! Hata hivyo, jambo
la kushangaza ni kwamba mamilioni ya watu wanaosoma Biblia hawaielewi!
Tunajuaje kwamba hawaielewi? Maisha ya watu hawa hayabadiliki na
kufuata maelekezo ya Neno la Mungu. Tatizo ni nini? Jibu tunalipata
katika MST. 17 “MTU AKIPENDA KUYATENDA MAPENZI YAKE (MUNGU), ATAJUA
HABARI YA YALE MAFUNZO“. Kama mtu hayuko tayari kulitenda kila jambo
atakalofundishwa na Mungu katika Neno lake, Roho Mtakatifu humwacha mtu
huyo, hawezi kumfunulia chochote katika Neno la Mungu. Matokeo yake
hawezi kuelewa lolote! Bila roho Mtakatifu hatuwezi kufunuliwa na
kulielewa Neno la Mungu (1 WAKORINTHO 2:10, 13; YOHANA 16:13). Wengi
wetu hatulielewi Neno kwa sababu hatuko tayari kulitendas. Hatua yoyote
ya kushindana na kupingana na Neno la Mungu, humfanya Roho Mtakatifu
kutuacha mara moja. Kabla ya kulisoma neno au kujifunza Neno la Mungu
kwa njia yoyote, ili tulielewe Neno la Mungu, hatuna budi kuwa na
msimamo wa kutaka kulitenda Neno lake sawasawa na (YEREMIA 42:1-6).
(2) JINSI YA KUMTAMBUA NABII WA KWELI (MST. 18)
Yeye anenaye kwa nafsi yake tu, huyo siyo nabii wa kweli. Kunena kwa
nafsi yake mtu, ni kuhubiri au kufundisha kinyume na Neno la Mungu. Mtu
wa jinsi hii, hatafuti Utukufu wa Mungu, bali wake mwenyewe. Nabii wa
kweli humhubiri Kristo, au kwa jinsi nyingine, hulihubiri Neno!
(WAFILIPI 1:18; 2 TIMOTHEO 4:2).
(3) KUSHINDWA KWA WANADAMU WOTE KUISHIKA TORATI (MST. 19)
Wanadamu wote mble za macho ya Mungu, hakuna hata mmoja aliyeweza
kuishika torati, maana mtu akiishika sheria yote, ila akajikwaa katika
neno moja, anahesabiwa kukosa juu ya yote (YAKOBO 2:10). Hivyo, mbele
za Mungu, hakuna mwanadamu atendaye mema, la, hata MMOJA! (WARUMI 3:10,
12; 1 YOHANA 1:8). Wanadamu wote tulistahili kuangikwa msalabani kama
adhabu ya laana ya kutokuishika torati (WAGALATIA 3:10; KUMBUKUMBU
21:22-23). Aliyempendeza Mungu sikuzote, na kufanya yaliyompendeza, ni
Yesu Kristo pekee (MATHAYO 3:17; YOHANA 8:29). Ni kwa sababu hii,
tunahesabiwa haki BURE kwa neema yake, kwa neema yake, kwa njia ya
ukombozi ulio katika Kristo Yesu kwa imani katika damu yake iliyomwagika
msalabani, alipokufa kwa niaba yetu, ili awe upatanisho (WARUMI
3:24-26; 1 TIMOTHEO 2:5-6).
(4) SABABU KUU YA KUMWITA MTUMISHI WA MUNGU KWAMBA ANA PEPO (MST.19-
20)
Mtumishi yeyote wa Mungu anayeyafichua maovu yaliyo……………………………. katika
jamii ya watu wanaojiita Wakristo, na kuyanena waziwazi kwamba
hayampendezi Mungu, na kuisema kweli, huyu sharti watu hao watamwita ana
pepo. Dhambi zinapokubalika katika Kanisa lote la Mungu na watu
wanaojiita Wakristo, wanapokuwa hawana tofauti na wapagani au mataifa,
anapoinuliwa Mtumishi wa Mungu na kuleta mageuzi, sharti mtu huyo
ataitwa ana pepo. Yesu hapa alifichua maovu yao na kuisema kweli kwamba
wanataka kumuua, wao wakakana, wakaipinga kweli hiyo wakati ilikuwa
kweli; kinyume chake wakamwita ANA PEPO, ili kujikosa na kuhalalisha
maovu yao! (MST. 19-20, 23). Hivyo ndivyo inavyokuwa wakati awote.
Haya yalimpata Martin Luther, John Wesley, Charles Finney na wote
walioleta mageuzi ya jinsi hii nyakati zao.
(5) WAJIBU NA JINSI YA KUHUKUMU (MST. 21-24)
“Ifanyeni hukumu iliyo haki“, ni mafundisho ya Yesu Kristo kwetu.
Hatupaswi kukaa kimya kwa visingizio vya Neno, “Msihukumu“, na kuacha
kuyakosoa mafundisho potofu ya Mashahidi wa Yehova; Mormonism au Christ
Church for Latter Day Saints, wanaoshika mafundisho ya Joseph Smith; au
wanaojiita Wakristo na kusema wao siyo dhehebu, wanaofuata mafundisho ya
William Branham; au mafundisho yanayofundisha watu kushika sabato leo,
au mafundisho mengine yoyote yaliyo potofu. Kukaa kwetu kimya na
kuogopa “kuyasema madhehebu mengine“, siyo kufuata nyayo za Mchungaji
Mkuu wa Kondoo, Yesu Kristo na kufanya hivyo, ni kuwaachia kondoo wetu
wararuliwe na mbwa mwitu. Huo ni uchungaji wa mshahara. Yesu aliifanya
hukumu iliyo haki, pale alipokuwa kinyume na kuishika Sabato, na tena
pale aliposema “Jilindeni na *chachu* au mafundisho ya Mafarisayo na
Masadukayo“. (MATHAYO 16:11-12; YOHANA 10:12; MATENDO 20:28-30).
Tunapaswa kufuata kielelezo cha Yesu. Kanisa la Kwanza walizingatia
kufanya hivyo (WARUMI 16:17; 2 YOHANA 1:9-11). Watu wenye mafundisho
potofu, hatupaswi kuwa na ushirika nao, tuwahesabu tu kama mataifa na
kuwahubiria kweli na kutokukubali kusikia chochote kutoka kwao.
(1) SABABU KUU YA WATU WENGI KUSHINDWA KUMPENDEZA MUNGU
(MST.25-29)
Tangu zamani za kale, sababu kuu ya watu wengi kushindwa kumpendeza
Mungu, ni watu hao kuacha kumwamini Yesu na kuokolewa, kwa kungoja
kwanza WAKUU WAMWAMINI (MST. 26). Wengine wanangoja kwanza baba na
mama, mume au kiongozi wao wa dini aokoke, ndiyo eti nao waokoke, na
wanafuata mafundisho yao tu kimkumbo. Huu ni mtego mkubwa wa Ibilisi.
Ukitengwa ugali mezani kila mtu huchukua tonge lake mwenyewe! Ndivyo
ilivyo, damu imemwagika msalabani, wokovu tayari. Kila mmoja anapaswa
kuuchukua kwa imani. Ni muhimu kukumbuka pia kwamba, kila mtu
atalichukua furshi lake mwenyewe na kutoa habari zake MWENYEWE
(WARUMI14:12; WAGALATIA 6:5). Hakuna haja ya kungoja wakuu waokoke
ndiyo nasi tuokoke. Kufa hakufuati nani wa kwanza kuzaliwa!.
(7) SAA YA KUKAMATWA (MST. 20).
Maadui zetu watatutafuta sana ili watushike na kutudhuru, hata hivyo,
hatupaswi kuhofu. Hatuwezi kufa mpaka saa yetu itakapowadia. Juhudi
zao zitagonga mwamba, wakati wote Bwana wetu atatupa mlango wa kutokea
maana amesema atakuwa pamoja nasi hat ukamilifu wa dahari yaani mwisho
wa mambo yote (MATHAYO 28:19-20; AYUBU 5:20, 26-27).
(8) NAMI NILIPO NINYI HAMWEZI KUJA (MST. 33-36)
Hatuwezi kumwona Yesu pasipo Utakatifu na kutafuta kwa bidii kuwa na
amani na watu wote (WAEBRANIA 12:14). Ni wale tu wenye mioyo safi
watakaomwona Mungu (MATHAYO 5:8). Ikiwa tumejaa masengenyo, chuki,
fitina, hasira, mawazo machafu, n.k. tutamtafuta Yesu tusimwone.
(9) MITO YA MAJI YALIYO HAI (MST. 37-44)
Mtu akimpokea Roho Mtakatifu, ishara ya kwanza itakayoonekana kwake, ni
kunena kwa lugha mpya kadri roho atakavyomjalia kutamka (MATENDO 2:4;
10:44-46; 19:6). Maji yanapokuwa yanapita katika mto, hutoa aina fulani
ya sauti isiyoweza kuelezeka. Ndivyo alivyo mtu anenaye kwa lugha
baada ya kumpokea Roho, mito ya maji hutoka ndani yake!
(1) KOSA LA KUMHUKUMU MTU KABLA YA KUMSIKIA KWANZA NA KUJUA
ATENDAVYO (MST. 31-32, 45-52)
Watu wengi hufanya kosa la kumhukumu Mtumishi wa Mungu kabla ya kumsikia
kwanza anenavyo au anavyofundisha na kujua atendavyo. Haitupasi
kufanya hivi. Watumishi waliotumwa na makuhani kumkamata Yesu,
walikubali kwanza kumsikia na wakagundua kweli waliyokuwa wamefichwa na
Shetani. Kuna faida kubwa kuiga mfano wao.
…………………………………………………………………………………………………………………………………. .
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA
12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO
WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu
ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa
kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata
rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko
tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi
fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante
kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili
kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.
Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe.
Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji
umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka
siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa
linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!
Bwana ametupa neema tena siku hii ya leo, kuendelea kujifunza Kitabu cha
YOHANA katika Biblia zetu. Leo, tutatafakari kwa makini YOHANA
8:48-59, na YOHANA 9:1-5. Kichwa cha somo letu la leo, “SABABU ZA
KUUGUA“, ni moja tu kati ya vipengele vingi vya somo letu. Tutaligawa
somo letu la leo katika vipengele saba:-
(1)KUVUNJIWA HESHIMA KWA MTUMISHI WA MUNGU (8:48-50);
(2)JINSI YA KUKWEPA MAUTI YA MILELE (8:51);
(3)YESU, MKUU KULIKO IBRAHIMU NA MANABII (8:52-58);
(4)KUJIFICHA KWA YESU (8:59);
(5)MTU KIPOFU TANGU KUZALIWA (9:1-3);
(6)SABABU ZA KUUGUA (9:3);
(7)KUZIFANYA KAZI ZA MUNGU MAADAMU NI MCHANA (9:4-5).
(1) KUVUNJIWA HESHIMA KWA MTUMISHI WA MUNGU (8:48-50)
Bwana wetu Yesu Kristo, hapa walimwita MSAMARIA, tena ANA PEPO.
Wasamaria walikuwa ni maadui wakubwa wa Wayahudi na walikuwa
hawachangamani kabisa (YOHANA 4:9). Wasamaria walihesabiwa kuwa ni
WAASI (HOSEA 13:16), na Msamaria yeyote alipoonekana hekaluni
Yerusalemu, walimpiga kwa “kipigo cha waasi“, na kumtoa nje ya hekalu.
Wasamaria walikuwa washirikina sana na uchawi ulikuwa jadi yao (MATENDO
8:9-11). Hivyo basi, Mafarisayo na Waandishi, walipomwita Yesu,
Msamaria; walikuwa na maana kwamba yeye ni adui wa taifa lao na dini
yao, tena ni mchawi anayestahili kupigwa “kipigo cha waasi“, na kutolewa
kati yao! Ilikuwa heri mtu alipoitwa MGALILAYA ambalo lilikuwa jina la
kuwabeza watu walio dhaifu, wanyonge, wasio na kitu! (YOHANA 7:52;
MARKO 14:70; LUKA 23:6). Mpaka leo, Wayahudi wanawaita Wakristo
“CUTHAEI“, kwa kuwabeza. Jina “CUTHAEI“, lina maana ya WASAMARIA! Yesu
hakuitwa tu Msamaria bali pia walimwita “ana pepo“ kwa maana kwamba ni
mwendawazimu, na hivyo hakuna haja ya kuyasikiliza maneno yake (YOHANA
10:20). Mafarisayo hawa, pia walisema Yesu anatoa pepo kwa nguvu za
mkuu wa pepo yaani shetani, hivyo walimwona ni Mtumishi wa Shetani na
siyo Mtumishi wa Mungu! (MATHAYO 9:32-34). Ni muhimu kwetu kujifunza
kwamba shetani atatumia watu wa namna zote hata Mafarisayo na Waandishi,
yaani viongozi wa dini kuvunja heshima ya Watumishi wa Mungu
wanaoihubiri kweli, ili watu wasiwasikilize. Paulo Mtume, aliitwa ana
wazimu alipoisema kweli, (MATENDO 26:24-25). Hata manabii wa zamani pia
waliitwa wana wazimu (2 WAFALME 9:1-11). Kanisa la Kwanza, kwa sababu
lilihubiri kweli, LILINENWA VIBAYA KILA MAHALI(MATENDO 28:22).
Hatupaswi kuona ajabu, Mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake. Yaliyompata
Yesu, yatawapata Watumwa wake waaminifu leo (YOHANA 15:20-21). Tukidumu
katika kweli lazima dhehebu letu litanenwa vibaya kila mahali, hizi ni
kazi za kwaida za shetani nyakati zote! Yesu alisema, “Mimi sina pepo,
lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu“.
Hapa hakujibu lolote juu ya yeye kuitwa Msamaria maana yeye ni MSAMARIA
MWEMA! Pamoja na Yesu kuvunjiwa heshima hivyo, hakuitafuta heshima
hiyo kwa nguvu kati yao! Heshima au utukufu wa kuutafuta mwenyewe, si
utukufu (YOHANA 8:54; MITHALI 25:27). Yesu alimwachia Baba kutafuta
utukufu wa kumpa, kati yao, na kuwahukumu yeye mwenyewe. Tunapovunjiwa
heshima, tusijisumbue kuitafuta heshima hiyo kwa watu, kwa nguvu zetu.
Tumwachie Mungu wetu kazihiyo, yeye huifanya vizuri sana kwa wakati
wake, tunapodumu kuwa waaminifu kuitenda kazi yake. Vivyo hivyo ni
muhimu kutambua kwamba wale wote wanaowaita Manabii wa Mungu kwamba ni
wapumbavu, wana wazimu, wana pepo n.k; watapatilizwa au kuhukumiwa kwa
maovu yao hayo (HOSEA 9:7).
(2) JINSI YA KUKWEPA MAUTI YA MILELE (8:51)
Jinsi pekee ya kukwepa mauti ya milele, ni KULISHIKA NENO la Mungu.
Kulishika Neno ni tofauti na kulisikia. Kulishika Neno maana yake
KULITENDA NENO (YAKOBO 1:22). Mtu anayelitenda neno la Mungu, hataopna
mauti milele. Maana yake nini maneno haya? Je, mtu akiokoka na kudumu
kulitenda Neno la Mungu, hatakufa kabisa? Jibu ni kwamba, watu
waliookoka, WANAKUFA kama watu wengine (WARUMI 8:36; 2 WAKORINTHO 4:11; 2
WAFALME 13:14; 2 TIMOTHEO 4:6). Kinachosemwa hapa na Yesu, ni kwamba
mtu anayelitenda Neno hataona MAUTI YA MILELE au MAUTI YA PILI yaani
hatatupwa katika ziwa la moto (UFUNUO 20:6; 21:8). Kufa kwa mtu
anayelitenda Neno ni kupita katika mlango wa uzima na kwenda kukaa
pamoja na Bwana Yesu (2 WAKORINTHO 5:6,8).
(3) YESU, MKUU KULIKO IBRAHIMU NA MANABII (8:52-58)
Ibrahimu alikufa, manabii wote walikufa, na makaburi yao yako hata leo.
Yesu aliye mkuu kuliko hao, Yeye alikufa na kufufuka siku ya tatu kama
alivyosema. Kaburi lake, liko wazi hivi leo (MATENDO 2:29-36; LUKA
24:3). Yesu Kristo alikuwako tangu zamani za kale, tangu milele, kabla
ya Ibrahimu, kabla ya vitu vyote (MIKA 5:2; WAKOLOSAI 1:17). YESU NI
MUNGU(1 YOHANA 5:20; TITO 2:13), hivyo hana baba, hana mama, hana
wazazi, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake (WAEBRANIA 7:3). Yesu
hakuanza kuwapo alipozaliwa na Mariamu. Katika MST. 54, Yesu anasema
“Anitukuzaye ni Baba yangu ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu“.
Watu hawa WALINENA TU kuwa ni Mungu wao, lakini ukweli hawakumjua Mungu
(1 YOHANA 2:3-5).
(4) KUJIFICHA KWA YESU (8:59)
“Wakaokota mawe ili wamtupie“. Waliokota mawe haya ili wamtupie, kwa
sababu alionekana kwao kwamba ANAKUFURU, kwa kusema kabla Ibrahimu
hajakuwako, yeye alikuwako, na kwamba Ibrahimu alishangilia kuiona siku
ya kuwako Yesu duniani. Kwa kuwaza hivyo, waliichukua sheria ya MAMBO
YA WALAWI 24:16 mikononi mwao. Yesu alijificha, akatoka hekaluni. Hapa
tunajifunza juambo la msingi. Hatupaswi kuwaacha watu watuonee wakati
tuna uwezo wa kujificha au kukimbia, kwa visingizio vya kukubali kuteswa
kwa ajili ya Kristo. Uzima wetu ni wa thamani sana kwa ajili ya
Injili. Mume ambaye hajaokoka anapotupiga na kutaka kutuua, hatuna budi
kujificha na kutoka nje!
(5) MTU KIPOFU TANGU KUZALIWA (9:1-3)
Baada ya Yesu kuvunjiwa heshima kiasi hicho, hakuacha kutenda kazi ya
Mungu au kubadili msimamo wake! Aliendelea kuitenda kazi ya Mungu kwa
msimamo wake uleule! Hii ndiyo siri ya kutumiwa sana na Mungu!
Vilevile wanafunzi wake hawakumwacha na kuona aibu kuambatana na
Mchungaji wao, aliyenenwa vibaya na kuitwa ANA PEPO! Ssisi nasi
tunapaswa kufuata mfano wa wanafunzi hawa. Kamwe tusione aibu
kuambatana popote na Mchungaji anayesemwa vibaya kila mahali, na
kuambiwa ana pepo au yeye ni pepo, wakati tuna hakika kwamba anafundisha
kweli. Hapa Yesu anakutana na mtu kipofu tangu kuzaliwa na
kutufundisha kwamba sisi sote ni vipofu tangu kuzaliwa kwetu kutokana
na dhambi zetu. Kipofu hutembea gizani na kuanguka shimoni pasipo
kupenda. Ndivyo alivyo mwenye dhambi yeyote. Mtu akikataa kwamba yeye
siyo kipofu hawezi kusamehewa dhambvi zake (YOHANA 9:39-41; ZABURI 51:5;
WARUMI 3:23; 1 YOHANA 1:8-10).
(6) SABABU ZA KUUGUA (9:3)
Wako watu wengine waliookoka ambao wakiona wake zao, waume zao au
wapendwa wengine wanaugua, huwaambia kwamba wanaugua kwa sababu
wametenda dhambi. Huku ni kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu na
kumtenda dhambi Kristo (1 WAKORINTHO 8:11-12). Hatupaswi kuhukumu
hivyo. Ziko sababu nyingi zinazoweza kumfanya mtu awe mgonjwa:-
Dhambi (ZABURI 38:3-4; YEREMIA 30:12-14; YOHANA 5:14);
Ili Mungu ajipatie utukufu kwa kumponya kwa muujiza (YOHANA 11:1-4);
Ili kazi za Mungu zidhihirishwe ndani ya mtu huyo (YOHANA 9:3);
Kutokana na KUONEWA na Ibilisi (MATENDO 10:38);
Kumpa Ibilisi nafasi kwa kushindwa kumpinga na kumkemea (WAEFESO 4:27; YAKOBO 4:7);
Upungufu wa Imani (MATHAYO 17:18-20; MARKO 6:5-6).
Ikiwa hatujatenda dhambi yoyote, hatupaswi kudanganywa na Ibilisi kwamba
ugonjwa uliotupata umetupata sababu ya dhambi. Zakaria na Elisabeti
walikuwa tasa, lakini walikuwa wenye haki mbele za Mungu bila lawama
yoyote (LUKA 1:5-7). Tukimruhusu Shetani atudanganye hivyo, mioyo yetu
hutuhukumu bure na kutukosesha ujasiri kwa Mungu, na hivyo maombi yetu
huwa hayapati majibu (1 YOHANA 3:21-22).
(7) KUZIFANYA KAZI ZA MUNGU MAADAMU NI MCHANA (9:4-5)
Giza linakuja, na wakati wa kulala utafika. Kama baba zetu walivyolala,
sisi nasi tutalala au kwa maneno mengine, tutakufa. Siku ya kufa
hatuijui. Tufanye kazi ya Mungu kana kwambaKESHO HAIKO. Hii ndiyo siri
ya kufanikiwa.
…………………………………………………………………………………………………………………………………. .
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA
12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO
WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu
ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la!
Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni
mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa
kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata
rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko
tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi
fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante
kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili
kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.
Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe.
Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji
umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka
siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa
linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!
0 comments:
Post a Comment